KOCHA MKUU WA MBEYA CITY, MMALAWI KINNAH PHIRI.
KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Mmalawi Kinnah Phiri amesema hakuna
wasiwasi wowote juu ya kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wa ufunguzi
wa duru ya pili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wageni
Kagera Sugar ya Bukoba mkoani Kagera.
Akizungumza jana kwenye mazoezi ya kikosi hicho yanayofanyia kwenye Uwanja wa shule ya Sekondari Igawilo, kocha Phiri alisema kuwa kutokana na sababu kadha wa kadha City ilichelewa kuanza mazoezi tofauti na timu zingine ambazo zilianza mapema ikiwemo Kagera Sugar, lakini hakuna shaka kuwa timu yake itaibuka na ushindi dhidi ya timu hiyo kutoka Kagera hapo Desemba 17 kwenye uwanja wa Sokoine.
“Najua tulichelewa kuanza mazoezi tofauti na wenzetu, leo tuna wiki moja kamili wengine wana zaidi ya hapo, ninazo programu maalumu kuhakikisha vijana wangu wanakuwa fiti kabisa, imani yangu kubwa kuwa tutaibuka na ushindi kwenye mchezo wetu wa kwanza Desemba 17, naifahamu timu hii iko imara kwenye kiungo, hilo nalifanyia kazi, hii ni duru ya pili ambayo inahitaji pointi tatu kwa kila mchezo ili kutimiza malengo,” alisema.
Katika hatua nyingine kocha Phiri alisema kwamba amesitisha mpango wa kutangaza nyota wapya aliowasajili katika kipindi hiki cha dirisha dogo, akisubiri kukamilishwa kwa mambo kadhaa na baada ya hapo atakuwa tayari kuwaweka hadharani, ambao ndani yake watakuwamo wanaotoka nje ya nchi pia.
“Tutakuwa na wachezaji wachache kutoka nje, lakini nitawajulisha baada ya muda, kwa sasa nimesitisha kidogo zoezi la kuwatangaza wachezaji wapya, kuna mambo kadhaa nataka yakamilike kwanza hivyo ni vyema mashabiki wetu watulie ila wajue tu kuwa timu imeimarishwa kwasababu tunataka kuwa na matokeo mazuri zaidi kwenye duru hii ya pili,” alisema.
No comments:
Post a Comment