asali

mbogo

sawe tv

advertise

SLIDE MANENO


Usipitwe na chochote, tupo ili kukuhabarisha tembelea blog hii kila siku, pia usisahau ku subscribe youtube channel yetu ya sawe tv

Wednesday, June 7, 2017

UKWELI WAZIDI KUIKABA KOO CCM,.. HATIMAYE PROF MUHONGO NAYE AKANYAGA NYAYO ZA NAPE,... TAZAMA HAPA MAZITO ALIYOFUNGUKA SIKU CHACHE BAADA YA KUTUMBULIWA


ALIYEKUWA Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema kwa sasa hatazungumzia kuondolewa kwake kutoka kwenye nafasi hiyo lakini amesisitiza kuwa “ukweli utabaki kuwa ukweli”.

Katika mazungumzo yake mafupi na Raia Mwema yaliyofanyika juzi Jumatatu, Muhongo aliwataka Watanzania watulie hadi pale ukweli utakapokuja kujidhihiri na kwamba yeye hana la kusema kwa sasa.

“Ahsante sana ndugu yangu kwa kunitafuta. Huwezi kupata lolote kutoka kwangu kwa sababu sitaki malumbano ila ukweli utabaki kuwa ukweli. Mimi sitaki malumbano ya aina yoyote,” alisema Muhongo.

Katika mazungumzo hayo, msomi huyo hakutaka kufafanua kuhusu ukweli huo ambao anaamini utabaki kuwa ukweli.

Profesa Muhongo, mmoja wa wasomi wabobezi katika masuala ya miamba duniani, alijiuzulu wadhifa wake huo wiki iliyopita, baada ya Rais John Magufuli kumtaka ajitathmini baada ya kutolewa kwa ripoti ya Kamati ya Profesa Abdulkarim Mruma.

Kamati ya Mruma ilipewa kazi ya kuchunguza makinikia yaliyokuwepo  katika makontena yaliyozuiwa kusafirishwa kutoka nchini na kwenda nchi za nje kwa ajili ya kufanyiwa uchenjuaji.

Baada ya uchunguzi huo wa takribani miezi miwili, kamati hiyo ilibaini kwamba makinikia hayo yalikuwa na madini ya dhahabu ya takribani tani 15 ambazo serikali ingeweza kupata mrabaha wenye thamani ya hadi shilingi trilioni 1.4.

Matokeo ya uchunguzi huo uliohusisha makontena 277 ya makinikia ndiyo yaliosababisha Rais Magufuli kutamka hadharani kwamba Muhongo anapaswa kujitathmini kama bado anafaa kuwa waziri na ikiwezekana ajiuzulu.

Barua ya kujiuzulu

Hata hivyo, jioni ya siku hiyo, Ikulu ilitoa taarifa ya Ikulu kutengua uteuzi wa Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini; lakini baada ya taarifa hiyo – takribani saa moja baadaye, mitandao ya kijamii ilisambaziwa barua ya kujiuzulu kwa Muhongo.

Katika barua hiyo, Muhongo hakukiri makosa yoyote katika jambo hilo lakini alieleza kwamba alitekeleza wajibu wake wote kama ambavyo alielekezwa na Rais Magufuli.

“Mheshimiwa Rais, napenda kukufahamisha kwamba nimejitahidi kufanya kazi kwa uwezo wangu wote kuitumikia Wizara ya Nishati na Madini tangu uliponiteua kuwa Waziri mnamo Desemba 12, 2015. Nakushukuru sana kwa miongozo yako ya kazi ambayo imenisaidia sana katika utekelezaji wa majukumu yangu ya kazi,” ilieleza barua hiyo iliyoandikwa Mei 24, 2017.

Baadhi ya wanasheria walioiona barua hiyo kupitia mitandao ya kijamii, walitafsiri maelezo hayo ya Muhongo kama ya kutokubali kukosea lolote isipokuwa kukubaliana na mamlaka ya uteuzi iliyomtaka aachie ngazi.

Wakati huo huo, wanasheria mashuhuri nchini wamesema huu ni wakati wa kumsaidia Rais Magufuli na serikali yake katika kuhakikisha kwamba utajiri wa maliasili uliopo Tanzania unanufaisha nchi na si mataifa yaliyowekeza hapa nchini.

Wanasheria hao wameonya kwamba Tanzania imesaini mikataba ya kimataifa ambayo kama haitaangaliwa vema, huenda taifa likapata hasara kubwa badala ya faida inayotarajiwa.

Makamu Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi, alisema suala alilolianzisha Magufuli la kupigania rasilimali za taifa halina vyama wala itikadi isipokuwa ni la kitaifa.

“Kwa maoni yangu, ningependekeza iundwe sasa tume ya wataalamu itakayojumuisha watu kutoka serikali ya Tanzania na kampuni za madini zilizopo nchini ili kwanza ukweli huu uwekwe wazi, baada ya hapo itakuwa rahisi kwetu kushitaki kwenye vyombo husika,” alisema Ngwilimi.

Kauli hiyo ya Ngwilimi iliungwa mkono na mmoja wa wanasheria maarufu nchini, Dk. Adelatus Kilangi, aliyesema kwamba kwa hali ilivyo sasa kwa kuzingatia mikataba ambayo Tanzania imeingia kimataifa, hatuwezi kuvunja mikataba ya madini iliyopo sasa kwa sababu ya ripoti ya Mruma.

“Hatuwezi kuivunja. Tumesaini mkataba wa MIGA na wa ICSID. Tutashtakiwa kwa kuvunja Customary Law Principle ya 'Fair and Equitable Treatment', na 'State Responsibility' na ya 'Respect for Acquired Rights'. Tutapelekwa mbele ya ICSID na kuhukumiwa, kisha tutaminywa na MIGA itakayokamata mali zetu popote zilipo.

“Kuwashtaki makampuni kwa kutudanganya? Tunaweza, na tutatumia hoja kuwa wamevunja Customary Law Principle ya 'Good Faith and Prohibition of Abuse of Rights'. Lakini wakisema uchunguzi wa mchanga tumeufanya kwa upande mmoja wanaweza kushinda. Ndiyo maana ni muhimu tufanye uchunguzi wa pamoja,” alisema Kilangi.

Katika andishi lake aliloliandika kwa jumuiya ya wanafunzi waliowahi kusoma katika Shule ya Sekondari ya Sengerema na ambalo baadaye lilisambazwa katika makundi mbalimbali ya WhatsApp hapa nchini, Kilagi alieleza kwa kina kuhusu changamoto za kisheria, kodi na utawala zilivyochangia nchi kufika ilipo sasa.

Kwa mfano, alisema ni wazi kuwa wakati nchi ikiingia kusaini baadhi ya mikataba ya rasilimali, taifa lilikuwa limetekwa na vikundi maslahi ambavyo vilikuwa vikifikiri kwa niaba ya serikali.

“Kuna tatizo kubwa sana linalozikumba hasa nchi za Afrika na baadhi ya zinazoendelea zilizo nje ya Afrika. Hili ni tatizo la 'state capture' (nchi kutekwa na vikundi maslahi). Kama ilivyo concept ya 'river capture' kwenye somo la jiografia, basi state capture linamaanisha ushawishi unaofanywa na watu wa kada ya juu, wafanyabiashara au wawekezaji kiasi kwamba serikali inashindwa kufikiri na kuachia kundi hilo kufikiri kwa niaba yake.

 “Wakati wa kufuata falsafa ya soko huria katika rasilimali, Tanzania iliingia kwenye utekwaji huu. Ndio kusema tuliondoa kichwa chetu tukaweka kichwa kingine. Tukawa tunafikiri kwa mfumo wa hicho kichwa kingine. Sasa tumeanza kurudisha kichwa chetu,” alisema.

Tanzania ilivyobanwa

Katika andishi lake hilo refu, Dk. Kilangi alieleza namna Tanzania ilivyozidiwa akili katika hatua za mwanzo za kuingia katika mikataba ya nishati na madini.

Kwa mfano, alitoa mfano wa madini ambapo wawekezaji walikataa kuweka sheria inayoruhusu nchi inayoibiwa utajiri wake kuomba kupitiwa upya kwa mikataba endapo kutakuwa na udanganyifu.

“Ili uweze kufanya mapitio ya mikataba, ni lazima kwenye mikataba tuliyoingia tuwe na kipengele kinachohusiana na doctrine ya 'clausula rebus sic stantibus. Hiki ni kipengele  kinachoruhusu kupitia upya mikataba kama mambo fulani yakibadilika.

“Lazima kifungu hiki kiwe kwenye mikataba. Hawa jamaa (wenye kampuni za madini) walihakikisha hakimo kwenye mikataba yetu. Kwa hiyo, ukianza mchakato wa kupitia mikataba mwenyewe bila ya kuwashirikisha wao watasema umevunja kanuni ya 'fair and equitable treatment'. Hivi ndivyo ilivyo,” aliandika mwanasheria huyo.

Kwa mujibu wa msomi huyo, tatizo hilo la kwenye madini lipo pia kwenye sekta ya nishati, ambapo wenye kampuni huwa tayari kuidanganya nchi kwa misaada wanayojua inahitajika sana; ikiwamo misaada ya wataalamu, lakini kumbe wanatengenezea sheria itakayowezesha kutuibia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT), Dk. Rugemeleza Nshala, alisema Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na mabadiliko yaliyofanyika mwaka 2015 ilitengenezwa kwa kufuata matakwa ya Benki ya Dunia (WB) na kampuni za madini zilizopo nchini.

Alisema kuna haja ya kufanya mapitio ya mikataba yote ambayo serikali iliingia na wawekezaji katika eneo la rasilimali kwa vile ilipitishwa na watendaji waliokuwa hawajui thamani ya madini hayo.

Nshala alishauri upitiaji wa sheria hii ujumuishe taasisi na wadau wote wa ndani ya nchi na iandikwe na Watanzania wenyewe na serikali ikatae msaada wa uandikaji wa muswada wa sheria hiyo kutoka Benki ya Dunia au mataifa yaliyoendelea kwa kuwa ajenda yao ni kuwa kampuni za nje ndizo zenye haki ya kuchimba na kunufaika na madini ya nchi husika.

“Uchimbaji na uchenjuaji wa Tanzanite pamoja na utengenezaji wa bidhaa za mwisho za madini hayo lazima ufanyike Tanzania. Kampuni kama Tiffany ziambiwe kuwa ni lazima waanzishe viwanda vya utengenezaji vito na mapambo yatokanayo na Tanzanite nchini. Hivyo nchi yetu ndiyo iwe duka la bidhaa za Tanzanite na si Marekani kama ilivyo sasa,” aliongeza.

LEAT ni mojawapo ya asasi za kiraia za kwanza kabisa nchini kupinga ubinafsishaji wa migodi ya madini uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Tatu na Nshala pamoja na aliyekuwa mwenzake katika taasisi hiyo, Tundu Lissu (sasa mbunge), waliwahi kufunguliwa mashitaka na serikali kwa sababu ya upinzani wao kwa sera hizo.

Kuhusu MIGA na ICSID

MIGA ni taasisi iliyo chini ya WB ambayo wawekezaji kutoka nchi zilizoendelea huweka bima kwa miradi yao ya uwekezaji wanayoifanya katika nchi masikini. Taasisi hii ilianzishwa mwaka 1965.

Endapo nchi inayoendelea kama Tanzania itavunja mkataba wake na kampuni hiyo, kampuni hiyo hupeleka kesi yake katika Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kiwekezaji (ICSID) na kama itashinda MIGA italipa fedha ambazo kampuni hiyo itadai kupoteza kutokana na uvunjwaji huo wa mkataba.

MIGA ikishalipa, kazi yake itakuwa ni kufuatilia kuona nchi husika inalipa fedha hizo na taasisi hiyo ina uwezo wa kukamata hata mali za nchi husika ilimradi nayo ilisaini mkataba wa kukubali MIGA


No comments:

Post a Comment

MAKTABA YA MAGAZETI / NEWSPAPER LIBRARY....... SOMA HAPA MAGAZETI YA SASA NA YALIYOPITA

  • MAGAZETI.
  • Tree in field with blue sky.
  • MAGAZETIt