Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia mkazi wa Olasiti, jijini
Arusha, Hamisi Amani (17), kwa tuhuma za kumuua mwenzake wakati
wakigombea soda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa
Arusha, Charles Mkumbo, tukio hilo lilitokea Desemba 25, mwaka huu, saa
mbili usiku katika eneo la Kwa Morombo. Kamanda Mkumbo alimtaja marehemu
kuwa ni Novatus Tadei (26), mkazi wa Kwa Mrombo na kwamba aliuawa kwa
kuchomwa kisu kifuani upande wa kushoto.
“Marehemu na mtuhumiwa walikuwa wapishi kwenye kampuni inayojulikana
kwa jina la ZZ Catering inayomilikiwa na Bashiri Ally. “Siku ya tukio,
marehemu pamoja na wafanyakazi wengine, akiwamo mtuhumiwa, baada ya
kumaliza kazi waliyokuwa wanafanya, walipanda gari lenye namba za
usajili T 375 CHH, aina ya Toyota Hiace wakirejea nyumbani”.
“Wakiwa ndani ya gari hilo, mtuhumiwa Hamis aligundua kuwa soda
aliyokuwa ameiweka ndani ya begi lake, haipo na kuanza kuhisi marehemu
ndiye aliyeichukua. Kwahiyo, ulizuka ugomvi baina yao na kuanza
kutukanana matusi. Wakati ugomvi huo ukiendelea, mtuhumiwa alimkaba
marehemu na kuchukua kisu wanachotumia kwenye shughuli zao za mapishi
kilichokuwa ndani ya vyombo na kumchoma kifuani, ” alisema Kamanda.
“Baada ya kuchomwa kisu, Tadei alianguka chini na jitihada za
wafanyakazi wenzake waliokuwamo ndani ya gari hilo kuokoa maisha yake
zilishindikana, kwani alifariki wakati anapelekwa hospitali kwa ajili ya
matibabu,” aliongeza Kamanda Mkumbo.
Aidha Kamanda huyo alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika
Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru na mtuhumiwa atafikishwa
mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi kukamilika
SLIDE MANENO
Wednesday, December 28, 2016
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment