Mapya
yameibuka sakata la kukwama kufungwa kwa ndoa ya Samwel Mwakalobo na
Ginen Mgaya, baada ya kubainika kuwa moja ya sababu ni Bibi harusi
mtarajiwa kuendeleza uhusiano na mzazi mwenzake.
Bwana harusi, Samuel Mwakalobo alitoweka muda mfupi kabla ya kufunga
ndoa na Ginen Mgaya katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Usharika wa Isanga jijini Mbeya.
Mwakalobo (26) alizua taharuki hiyo Ijumaa ya Desemba 16, baada ya
kutoonekana kanisani kufunga ndoa mbele ya Mchungaji Andagile
Mwakijungu.
Habari
zimedai kuwa kabla ya mpango wa kufunga ndoa hiyo, Mgaya tayari
alishapata mtoto kabla hajaolewa, na Bwana harusi kubaini dakika za
mwisho kuwa wawili hao walikuwa bado wana uhusiano wa karibu.
Habari
hizo za ndani kutoka familia ya Bibi harusi, zilidai kuwa kilichofanya
Bwana harusi amtelekeze Bibi harusi ni wasiwasi aliokuwa nao juu ya
uhakika wa ujauzito wa mkewe huyo mtarajiwa, kuwa ni wake kweli au wa
mpenzi wake huyo wa zamani.
“Hofu
hiyo ilijengeka kutokana na taarifa alizoziamini Bwana harusi kuwa Bibi
harusi anaendeleza uhusiano na mzazi mwenziwe. Ni hofu tu ambayo
angeifanyia kazi na angegundua kuwa haina ukweli wowote,” kilidai chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliendelea kudai:
“Unajua muda mwingine binadamu tunahitaji kufanya uamuzi kwa kutafakari
… maana shemeji yetu (Bwana harusi) alipigiwa simu na mzazi mwenza wa
Bibi harusi na kuelezwa maneno ya ‘shombo’ na yeye bila kufanyia
utafiti, akaamua kususa harusi.”
Wakati
taarifa hizo zikibainisha hayo, familia ya Bwana harusi imeendelea
kufanya jitihada za kuhakikisha suala hilo linamalizika kistaarabu.
Anayeelezwa
kufuatilia suala hilo kwa karibuni ni kaka yake, ambaye hadi jana
jitihada za kumtafuta mdogo wake zilikuwa zimeshindikana kutokana na
kutopokea simu yake ya mkononi mara zote.
“Anayeongoza
familia ya Bwana harusi ni kaka yake. Inasemekana pia kuwa wawili hao
waliingia kwenye mgogoro dakika za mwisho kabla ya harusi na ndiyo maana
baada ya kutoweka hataki hata kupokea simu,” kilieleza chanzo kingine.
Awali,
mpambe wa Bibi harusi alieleza kuwa siku mbili kabla ya harusi hiyo,
Bwana harusi alikuwa kwenye migogoro ya kifamilia na ndugu zake kuhusu
fedha za sherehe na mpaka siku ya sherehe, suala hilo walikuwa
hawajalitatua.
“Lakini
tunashukuru kaka yake ni mstaarabu, aliamua kuonesha upendo kwa mdogo
wake na amekuwa akilifuatilia suala hilo ili limalizike kwa amani,
lakini mdogo mtu hapatikani,” alisema mpambe huyo.
Alisema
jitihada za Bibi harusi kumtafuta Bwana harusi hazijazaa matunda, kwani
hadi juzi alikuwa hapatikani hata nyumbani kwake, ingawa redio ilikuwa
inasikika ndani ya chumba hicho kilichofungwa kufuli kwa nje.
Simu
ya Bwana harusi ilikuwa ikiita muda mwingi bila kupokewa, lakini hatua
zingine zilidai kuwa Bwana huyo ambaye ni mfanyabiashara kwenye kituo
cha mabasi yaendayo Chunya eneo la Isanga jijini Mbeya hajafungua duka
lake.
No comments:
Post a Comment