WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amesema uwezekano wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kushinda katika uchaguzi wilayani Arumeru, mkoani Arusha ni mdogo.
Amesema hali hiyo inatokana na uamuzi wa vyama hivyo kila kimoja kusimamisha mgombea udiwani katika Kata ya Matevesi, kinyume na makubaliano.
Lowassa alisema hayo katika kampeni za kumnadi mgombea udiwani wa kata hiyo. Alisema kilichofanywa na vyama vya upinzani ni kugawa kura, wakati upinzani ulikuwa na nafasi kubwa ya kushinda.
Alisema vyama vinavyounda Ukawa vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi, kila kimoja kimesimamisha mgombea udiwani katika kata hiyo, kwa hali hiyo uwezekano wa kushinda ni mdogo sana, hivyo kukipa mwanya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushinda kiti hicho.
Akizungumza katika kampeni za Chadema zilizofanyika katika Kitongoji cha Ematasia, Lowassa alisema vyama hivyo tayari vimeshafanya kosa la kiufundi, linaloweza kusababisha vyama hivyo ‘kuangukia pua’ katika uchaguzi huo na kuiwezesha CCM kuibuka na ushindi asubuhi na mapema.
Alisema CCM ina nafasi kubwa ya kushinda katika uchaguzi huo, kutokana na kuwa na uhakika wa kura zake, kutokana na kutokuwa na upinzani wa chama kingine chenye mrengo wake, kama ilivyo kwa vyama hivyo vya Ukawa, ambavyo viko katika hatari ya kugawa kura.
“Nyie tayari mmeshafanya makosa makubwa ya kiufundi kwa kila chama cha Ukawa kusimamisha mgombea wake, hapo ndipo CCM wanaposhindia, kwa hiyo mwendelee mkijua mna kazi kubwa kushinda,” alisema Lowassa.
Katika hali ya kushangaza Lowassa alijikuta akimuombea kura mgombea wa CCM, Julius Savoyo aliposema wananchi wa kata hiyo wanapaswa kumpa kura na kumuweka madarakani mgombea aliyeshinda katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2015, pasipo kujua diwani aliyeshinda wakati huo na kutenguliwa na mahakama ni wa CCM.
“Wananchi wa kata hii hamna kazi ngumu katika uchaguzi pamoja na makosa yaliyofanywa na vyama vya Ukawa, hakikisheni mnamrejeshea udiwani yule aliyeshinda wakati ule ili aendelee na kazi yake,” alisema Lowassa.
Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Shaaban Mdoe alisema kitendo kilichoonekana na Lowassa kuwa ni kosa kusimamisha wagombea wa vyama vya Ukawa ni utabiri mzuri wa ushindi kwa CCM, kama alivyosema tena katika kampeni za uchaguzi wa Urais mwaka juzi.
Hata hivyo, Mdoe alisema suala la Ukawa kwa sasa halipo tena, bali ni Ukiwa na ndiyo maana kila chama cha muungano huo, kinajaribu bahati yake kutokana na kuvunjika kwa ndoa hiyo ; na wa mwisho kuondoka katika ndoa hiyo, alikuwa ni Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Mdoe alisema kitendo cha Lowassa kumnadi mgombea wa CCM, si bahati mbaya bali ni ukweli uliopo ndani ya moyo wake, kwa kuwa hata akijifungia chumbani kwake peke yake, anakubali kazi nzuri inayofanywa na serikali ya Rais John Magufuli
No comments:
Post a Comment