Meneja wa Simba Musa Hassan Mgosi amesema, benchi la ufundi la Simba limefarijika kusikia na kuona wachezaji wengi wa kikosi chao wakiitwa kwenye timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), kwa ajili ya michezo ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Botswana na Burundi ambayo itafanyika baadae mwezi huu.
“Hiyo ni faraja kwa sababu kwa sasa timu ambayo ipo kwenye mstari na wachezaji wake wako vizuri kisaikolojia na hawana stress ni Simba pekeyake. Kwa sababu kuna timu nyingine ambazo mashabiki wake wana stress ambazo zinaingia hadi kwa wachezaji kwa hiyo huwezi kupata matokeo kwa sababu wachezaji hawajatulia.”
Mgosi pia amezungumzia kuhusu mbio za ubingwa wa msimu huu ambapo amesema: “Hawakuangalia kuifunga Yanga pekee bali waliangalia mechi 10 za mbele yao kabla ya kumaliza ligi ikiwemo mechi ya Simba na Yanga, bado tunahitaji kuendelea kushinda mechi zetu na kupata pointi tatu ili kupata kile tunachokihitaji ambacho ni ubingwa. Hatuwezi kupata ubingwa kama tutashindwa kushinda mechi zetu zilizo mbele yetu.”
Wachezaji wa Simba walioitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ni Jonas Mkude, Said Ndemla, Shiza Kichuya, Mohamed Hussein, Abdi Banda, Mzamiru Yassin na Ibrahim Ajib.
No comments:
Post a Comment