Baada ya kulitema Kombe la FA, nahodha msaidizi na kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, amewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo akiwaambia kuwa ni lazima wauchukue ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Niyonzima raia wa Rwanda alitoa kauli hiyo jana Ijumaa asubuhi baada ya mazoezi ya timu yake ambayo leo Jumamosi inacheza na Prisons ya Mbeya mechi ya ligi kuu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 56, inacheza mechi hiyo ikitoka kufungwa bao 1-0 na Mbao FC katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Niyonzima alisema malengo kati yao na viongozi wa benchi la ufundi ni kushinda mechi zote tano walizobakisha ili wajiweke katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa.
Niyonzima alisema kingine wanachokitaka ni kuweka rekodi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu kwa mara ya tatu mfululizo.
“Tunaanza kwa kutopoteza mechi dhidi ya Prisons ambayo naamini ni ngumu, lakini tutapambana kadiri tuwezavyo ili kufanikisha malengo yetu, mashabiki watulie huu ubingwa ni wetu.
“Tunataka tuweke historia kwa kuchukua ubingwa wa ligi kuu kwa mara tatu mfululizo, ndiyo maana tunataka kushinda mechi zote zilizobaki,” alisema Niyonzima.
SOURCE: CHAMPIONI
No comments:
Post a Comment