WEKUNDU wa Msimbazi Simba wamejibu mapigo kwa wapinzani wao wa jadi, Yanga baada ya kumtaja beki wao mahiri, Kelvin Yondani na kiungo Haruna Niyonzima ambao mikataba yao inaelekea ukingoni.
Simba wamefanya hivyo kama sehemu ya kujibu mapigo kwa wapinzani wao hao ambao kila kukicha wamekuwa wakiwataja wachezaji wao mahiri, kiungo Jonas Mkude na mshambuliaji Ibrahim Ajib ambao nao wanamaliza mikataba.
Akizungumza na BINGWA, Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, alisema wapinzani wao Yanga waache kuwatoa kwenye reli ya ubingwa kwa sasa kwa kutaja nyota wao wanaotaka kuwasajili.
Alisema Yanga wanatakiwa kuwazungumzia nyota wao 14 wanaomaliza mikataba, akiwamo Haruna Niyonzima na Kelvin Yondani akidai kuwa ndio wenye uwezo wa kuichezea Singida United iliyopanda Ligi Kuu msimu huu.
“Kimsingi hata kifikra utaona kuwa si Yanga wala Singida United wenye uwezo wa kuwasajili akina Ajib, Mkude na Said Ndemla kwa kuwa tumeshamalizana nao, lakini pia tambua fika hawa hawawezi kwenda kucheza timu ya porini,” alisema Kaburu.
Alisema ni ngumu kwa nyota hao hivi sasa kuikacha Simba na kwenda kusaini Singida United kama ilivyokuwa ikiandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari na kusisitiza kuwa bado wataendelea kukipiga kwa Wekundu hao wa Msimbazi.
Hatua ya nyota hao kutajwa katika usajili wa Singida United inakuja ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo ipande Ligi Kuu na kupanga huku wakionekana kuwa na mikakati kabambe ya kutaka kuzinasa saini za wachezaji wengi nyota wa Ligi Kuu Bara, wakiwamo Ajib na Mkude.
No comments:
Post a Comment