KUMEKUWA na taarifa za mambo mbalimbali kuhusiana na bilionea namba moja Afrika kwa upande wa vijana, Mohamed Dewji kuamua kusitisha mchakato wake wa kutaka kununua hisa asilimia 51 Simba.
Imeelezwa kuwa, uamuzi wa Dewji maarufu kama Mo kuamua kusitisha mchakato huo ni baada ya baadhi ya viongozi wa Simba wakiongozwa na Rais, Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kuamua kufanya maamuzi bila ya kuwashirikisha katika suala la kuingia mkataba na kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa.
Simba imeingia mkataba wa miaka mitano na SportPesa na itapata jumla ya Sh bilioni 4.9 kwa miaka mitano. Mkataba unaonyesha kila mwaka watapata zaidi ya Sh milioni 800 lakini kila mwaka itakuwa ikiongezeka asilimia 5 na kufanya katika mwaka wa mwisho, Simba kupata Sh bilioni 1 na milioni 80.
Lakini kuanzia jana usiku, kumekuwa na taarifa kuwa Mo Dewji ameitaka Simba imlipe fedha zake Sh bilioni 1.4 ambazo amekuwa akitoa kwa ajili ya mshahara kupitia makubaliano ya kukopesha.
Hakuna aliyekuwa amethibitisha taarifa hizo hadi jana asubuhi, jambo ambalo lilizidi kuzua mkanganyiko huku baadhi ya mashabiki wakionekana kuwa na jazba, wako wakiuunga mkono uongozi na wengine wakiupinga na kudai haujamtendea haki Mo Dewji.
Juhudi za kumpata Mo Dewji kuhusiana na suala hilo kwa kuwa kuingia mkataba na kupata mtu wa kulipa mishahara ni jambo zuri sana. Vipi yeye akasirike na alikuwa anakopesha?
SALEHJEMBE NA MO DEWJI WALIFANYA MAZUNGUMZO NA YALIKUWA HIVI
SALEHJEMBE: Tumesikia umetaka kulipwa fedha zako Sh bilioni 1.4 ukiwaandikia Simba wafanye hivyo, mara moja, nini kimekuudhi?
Mo Dewji: Kwanza sijawaandikia, lakini wao wamenipigia na kunieleza wamepata mdhamini, wamepata fedha na watanilipa fedha zangu, nikasema hewala.
SALEHJEMBE: Kupata mkataba na SportPesa ni jambo zuri, kipi kinakuchukiza?
Mo Dewji: Sijachukizwa na kitu.
SALEHJEMBE: Labda fafanua, hizi fedha unazodai ni zipi wakati ilikuwa ikielezwa kwamba unasaidia?
Mo Dewji: Kila kitu kipo clear (wazi), uongozi unajua ninawadai, nimekuwa nikiwapa fedha za mishahara kila mwezi na huu ulikuwa mkopo. Lakini zaidi ya Sh milioni 500 nimetoa kama shabiki tu, nimesaidia kwenye bonus na mambo mengine mbalimbali. Hizo si deni, badala yake ni msaada kama shabiki na mwanachama wa Simba.
SALEHJEMBE: Kuna taarifa umechukizwa na umeamua kujitoa kuendelea na ule mchakato wa mabadiliko Simba?
Mo Dewji: Nimeamua kufikia uamuzi huo si kwa kuwa nina shida na hao SportPesa. Kwanza ni watu ambao siwajui kabisa, lakini kilichofanywa na viongozi wa Simba nimeona ni jambo linalokiuka urafiki, undugu, usemakweli na transparence (uwazi).
SALEHJEMBE: Kivipi wakati kila kitu kimeshughulikiwa sahihi?
Mo Dewji: Sahihi kivipi? Wakati tukiwa katika mchakato wa mabadiliko, tulikubaliana nitafute mdhamini. Nilikuwa katika mchakato na alikubali kwamba angeingia kudhamini mara tu baada ya mabadiliko kupitishwa. Sasa kama nilitumia nguvu yangu kumshawishi, leo vipi viongozi wanafanya hivi?
SALEHJEMBE: Labda waliona mdhamini wako anachelewa?
Mo Dewji: Kachelewa vipi, kasema baada ya kupitishwa kwa mchakato wa mabadiliko. Angekuwa anatoa takribani Sh bilioni 2 kwa mwaka, wao wanajua. Vipi wafanye mambo bila ya kunieleza sahihi, kuwaeleza wajumbe wa kamati ya utendaji?
SALEHJEMBE: Kuna taarifa ulipigiwa simu, ukaelezwa?
Mo Dewji: Lazima tutofautishe, nilipigiwa simu na Aveva, ilikuwa Alhamisi, akaniambia wanataka kuingia mkataba na SportPesa. Nikamuambia sawa, basi tukutane Jumamosi ili kuona wanatupa nini na nini, akakubali.
SALEHJEMBE: Mlikutana?
Mo Dewji: Tulikutana wapi, wamesaini mkataba Ijumaa, mimi niko kwenye gari dereva wangu ndiye alinionyesha. Aliniambia Simba wametoka vyumbani wakiwa na jezi za mdhamini mpya, nikamuambia ni jambo ambalo haliwezekani. Akanionyesha picha, hakika nilishangaa sana. Lakini hata baada ya kuwapigia wajumbe zaidi ya watatu wa kamati ya utendaji, pia hawakuwa wakijua.
SALEHJEMBE: Hawakuwa wakijua kuwa wamesaini mkataba, kamati ya utendaji walikutana Alhamisi, siku moja kabla ya mkataba!
Mo Dewji: Ni kweli walikutana, lakini wajumbe wengi hawakuwepo. Nimeambiwa Hans Poppe, Magori na wengine hawakuwepo.
SALEHJEMBE: Sasa unaondoka, nani ataendeleza ule mchakato?
Mo Dewji: Mimi acha historia inihukumu, yeyote aje. Wakati naondoka mwaka 2003, niliwaambia historia itanihukumu, baada mabadiliko niliyotaka yalikataliwa. Leo umeona kila mtu anataka kile nilichokisema mwaka 2003.
Mo Dewji: Mimi nabaki kuwa mwanachama mwaminifu kama nilivyofanya baada ya kuondoka 2003. Unaweza vipi kubaki na watu ambao hamuaminiani? Vipi mtajenga familia bora kama hamuaminiani, mnafichana mambo na inaonekana wengine wanafanya mambo si kwa faida ya klabu?
SALEHJEMBE: Wanasimba wengi, ninaamini wangependa ubaki.
Mo Dewji: Hata mimi ningependa hivyo, ndiyo maana naendelea kubaki ndani ya Simba kama mwanachama kwa kuwa viongozi wanaonekana wana malengo tofauti.
No comments:
Post a Comment