Kocha Mkuu wa Singida United, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, amesema hakuna mazungumzo yoyote yanayoendelea kati yao na wachezaji wa Simba, kiungo Jonas Mkude na mshambuliaji, Ibrahim Ajibu.
Pamoja na Pluijm kutotaka kuweka mambo yote hadharani lakini kuna taarifa tayari kuna jambo dhidi ya nyota hao wa Simba na kuna dau limeandaliwa kuwashawishi.
Wachezaji wengine wanaotajwa kusajiliwa na Singida msimu ujao wa ligi kuu ni Atupele Green anayekipiga Ndanda FC na kiungo fundi wa Yanga, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.
Pluijm amesema muda wa usajili bado, hivyo ni mapema kuzungumzia katika kipindi hiki na hizo taarifa zinazoenea za kumsajili Mkude na Ajibu ni tetesi pekee.
Pluijm alisema, bado hajaanza kazi rasmi ya kukisuka kikosi hicho na mara atakapoanza, basi haraka ataweka wazi mipango yake yote ikiwemo ya usajili. Hata hivyo, tayari usajili wa Singida United umeanza na wameshanasa takriban nyota watatu wakiwemo wa kimataifa.
"Ujue nimeikuta Singida ikiwa tayari ina wachezaji ambao wameipandisha kucheza ligi kuu, hivyo ni lazima niwape nafasi hawa niliowakuta kwanza kabla ya kuanza usajili wa wachezaji wapya.
"Na kingine mimi bado sijaanza kazi rasmi, hivyo nisubirie tuanze kwanza, halafu kila kitu ntakwambia, ni ngumu kuweka mipango yangu nikiwa bado sijaanza kazi.
"Hizo taarifa za kuwasajili wachezaji hao bado siyo rasmi, ni tetesi pekee, licha ya kutoa mapendekezo kwa uongozi wangu," alisema Pluijm.
No comments:
Post a Comment