Mafinga. Utata umeibuka kuhusu kusimamishwa Diwani wa Kata ya Boma (Chadema), Julits Kisoma kuhudhuria vikao vya Baraza la Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwa tuhuma kwamba hajui kusoma na kuandika.
Habari zilizothibitishwa na Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani, Charles Mkoga zimedai Kisoma amesimamishwa kujihusisha na shughuli za udiwani kwa tuhuma za kutojua kusoma na kuandika hadi hapo watakapopata maelekezo kutoka Ofisi ya Rais, Tamisemi na Tume ya Maadili ambako wamefikisha suala hilo.
Hata hivyo, Kisoma ameibuka na kukana madai ya kutojua kusoma na kuandika na kueleza kuwa anasubiri barua ili achukue hatua stahaki dhidi ya hicho kinachoendelea.
Pia, diwani huyo ametetewa na katibu wa madiwani wa Chadema, Georgina Kiduga aliyesema anajua kusoma na kuandika na kwamba anachofahamu diwani huyo hakuhudhuria vikao kutokana na kuumwa.
“Taarifa za mimi kusimamishwa nimezisikia. Niseme tu zinaniumiza kichwa sijajua ni kwa nini lakini ukweli ni kwamba sikuhudhuria kikao kimoja tena nilituma ujumbe wa simu ya mkononi kwa mwenyekiti wa baraza la madiwani. Pia nilimpigia simu nikimueleza kuwa sitafika kikaoni kutokana na hali yangu ya kiafya na nilikwenda kuhudhuria matibabu,” alisema Kisoma.
“Lakini niliporudi nilitumiwa barua iliyonitaka kuhudhuria kikao cha kamati ya maadili. Nilikwenda kule na kushindwana nao kutokana na hoja kubadilika kutokana na kile walichokuwa wameniitia na walichokuwa wakinihoji,” alisema.
Awali, akifafanua sababu za kusimamishwa kwa diwani huyo, Mkoga alisema hatua iliyolifanya baraza hilo kuamini kuwa uvumi uliodumu kwa muda mrefu kuwa diwani huyo hajui kusoma na kuandika ulitokana na kitendo chake cha kutohudhuria vikao vitatu vya madiwani
No comments:
Post a Comment