Mgogoro
wa uongozi unaoendelea ndani ya chama cha CUF huenda ukaathiri ushiriki
wake kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Januari 27 baada ya
pande zote mbili zinazosigana kujiandaa kuteua wagombea.
Mbali
ya mgogoro huo kuhofiwa kukiathiri chama pengine hadi kusababisha
wagombea wake kuzuiwa, pia unaweza kuudhoofisha Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa).
Habari
kutoka ndani ya chama hicho zinasema upande wa Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Msajili wa vyama vya siasa uko
kwenye maandalizi ilhali ule wa Katibu Mkuu, Seif Sharrif Hamad
unatarajiwa kukutana na watendaji wa chama kujadili ushiriki wao.
Profesa
Lipumba aliyeiongoza CUF tangu mwaka 1995, alijiuzulu kwa hiari
uenyekiti wake Agosti 2015 lakini siku chache kabla ya CUF kuitisha
mkutano Agosti mwaka huu wa kujadili barua yake, aliandika barua ya
kutengua kujiuzulu na akarejea kazini.
Siku
ya mkutano mkuu uliofanyika Ubungo Plaza, wajumbe waliridhia kujiuzulu
kwake lakini walipoingia kuchagua mrithi wake, wafuasi wa Profesa
Lipumba walivamia mkutano na kuuvuruga hali iliyosababisha baadaye
kusimamishwa kwake.
Alipoulizwa
jana namna CUF yenye mgogoro itakavyoshiriki uchaguzi wa madiwani
katika kata 22 Bara na ubunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar, Kaimu
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro alisema wapo katika
mikakati kuhakikisha wanashiriki kikamilifu.
Mtatiro
alisema muda wowote kuanzia sasa Katibu Mkuu, Maalim Seif atakutana na
watendaji wa chama kujadili kwa kina suala hilo na kutoa maelekezo.
“Tutashiriki
vizuri na niwaweke wazi Watanzania kuwa shughuli za chama zinaendelea
kama kawaida hivyo kamati za utendaji zitatimiza wajibu wake wa
kuwapitisha wagombea watakaojitosa kwenye kinyang’anyiro,” alisema.
Kuhusu
Profesa Lipumba, Mtatiro alisema, “Hatuwezi kufanya kazi na mtu wa CCM
kumsogeza karibu yetu ni kumleta atuharibie chama jambo ambalo hatuwezi
kuliruhusu. Ingekuwa lile suala la kujiuzulu aliteleza tungemwelewa na
kumsamehe lakini inavyoonekana yupo kwenye mipango yake katu hatuwezi
kumuweka karibu.”
Lakini
Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF anayemuunga mkono Lipumba,
Abdul Kambaya alisema, “Tuna kikao leo (jana) upande wa Bara chini ya
Mwenyekiti Profesa Lipumba kujadili suala hilo la uchaguzi, kuhusu
upande wa Zanzibar sifahamu chochote.”
Akizungumzia
uchaguzi huo mdogo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema upande wa Zanzibar,
Salum Mwalimu alisema Ukawa utakuwa bega kwa bega na CUF katika uchaguzi
huo kwani wanaitambua kuwa iko moja si mbili kama inavyotengenezwa na
watu wasiopenda maendeleo ya chama hicho.
“Tunatambua
na kuheshimu uamuzi wa wanachama na viongozi halali wa chama, CUF iko
moja, kama kuna mtu anatengeneza propaganda alifanya hivyo akiamini
anakwenda kukiua chama ajue bado kinaendelea kusimama,” alisema.
“Pale
atakaposimamishwa mgombea kutoka chama hicho Ukawa tutamuunga mkono na
kumpigania kuhakikisha anashinda. Tunaamini pia nao watafanya hivyo
akisimamishwa mgombea wa Chadema, ”alisema Mwalimu
Katibu
Mkuu wa NCCR-Mageuzi Juju Danda alisema mgogoro wa CUF hautaleta
changamoto yoyote kwenye Ukawa kwa kuwa wanamtambua katibu mkuu. Alisema
Ukawa unamtambua Maalim Seif na ndiye mtendaji mkuu wa chama hivyo
watakuwa tayari kushirikiana naye katika kila jambo.
Kuhusu
mpasuko unaoendelea ndani ya chama hicho, Danda alisema suala hilo
waachiwe CUF wenyewe ndiyo watakaoamua. “Mtendaji Mkuu wa chama ni
katibu si Mwenyekiti, na kwa kuwa tupo pamoja na Maalim hatuoni
changamoto yoyote yeye ndiye anayesimamia uteuzi na tunategemea mambo
yatakwenda sawa,” alisema.
Katika
hatua nyingine hatima ya Jaji Sekieti Kihiyo anayesikilkiza kesi ya CUF
kujitoa sasa itajulikana Desemba 14 atakapotoa uamuzi wa maombi ya
wadai kumtaka ajiondoe.
Jaji
Kihiyo alipanga kutoa uamuzi wa maombi hayo dhidi yake jana baada ya
kumaliza kusikiliza hoja za pande zote katika kesi hiyo, ambazo zilizua
mvutano mkali baina ya mawakili wa wadai kwa upande mmoja na mawakili wa
wadaiwa pamoja na Jaji Kihiyo kwa upande mwingine.
Kesi
hiyo imefunguliwa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamnini wa CUF,
dhidi ya Profesa Lipumba, Naibu Katibu Mkuu wa chana hicho Bara,
Magdalena Sakaya pamoja na wanachama wengine tisa waliosimamishwa
uanachama wa chama hicho.
Wengine
ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, ambaye ndiye
mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
ambaye ni mdaiwa wa pili.
Kesi
hiyo ilitarajiwa kusikilizwa jana lakini kabla ya kuendelea, kiongozi
wa jopo la mawakili wa wadai, Juma Nassoro aliieleza mahakama kuwa wadai
wameandika barua wakimtaka jaji ajiondoe kuendelea na kesi hiyo kwa
maelezo hawana imani naye.
No comments:
Post a Comment