HUWEZI kuwataja viungo watano bora wa miaka yote kwenye klabu ya Yanga bila ya kulitaja jina la Athumani Iddi ‘Chuji’.
Chuji ni moja ya viungo bora wakabaji kuwahi kutokea Tanzania na Afrika Mashariki na Kati. Ubora wake, kujituma na bidii alizozionesha uwanjani ndizo zilizomfanya aonekane bora kila siku.
Sahau kuhusu umri wake, kiungo huyu wa ulinzi na amepitia vipindi vingi vigumu katika maisha yake ya soka lakini alihakikisha anaonyesha kiwango cha hali ya juu kwenye klabu zake alizozitumikia hususani Yanga.
Alianza soka katika timu ya Polisi Dodoma, 2005, Chuji alitokea kuwa mlinzi bora wa kati katika soka la Tanzania, alikuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika timu ya taifa ya vijana ‘ Serengeti Boys’ mwaka huo, akitokea timu za nje ya Dar es Salaam.
Kupata nafasi ya moja kwa moja katika timu ya taifa ukitokea mkoani, bila shaka wewe utakuwa mchezaji ‘usiyegusika’ popote pale nchini.
Polisi Dodoma ndiyo timu iliyomfanya Chuji akaonekana kuwa mchezaji bora na kuanza kucheza klabu kubwa nchini.
Namba sita mwenye sifa za utulivu, mpangaji mzuri wa ngome na kiongozi mwenye kujiamini, ni sifa ambazo zilimfanya Chuji kusajiliwa na Simba, kwa ajili ya msimu wa mwaka 2006.
Chuji, aliingia Simba na kukuta wachezaji wengine wazuri kama yeye. Katika nafasi ya ulinzi wa kiungo wa kati ambayo alikuwa akicheza katika timu ya Polisi Dodoma, ndiyo alicheza nayo Simba.
Chuji, alitumia mwanya wa matatizo ya kinidhamu yaliyopelekea baadhi ya wachezaji muhimu kuwa kando ya timu. Costa, hakuwa na maelewano mazuri na kocha Neidor dos Santos, hapo ndipo Chuji alipata nafasi ya kuonesha kile atakacho.
Dos Santos, alipendezwa na viwango vya wachezaji vijana wakati huo, Chuji, Henry Joseph na Kelvin Yondan na akaamua kuwapatia nafasi ya kudumu kikosini hapo.
Soka la uhakika akicheza katika idara ya kiungo kwa dakika 120 lilimtambulisha kiungo, mwenye mapafu ya ‘ mbwa’ katika soka la Tanzania.
Chuji alihamia Yanga huku mashabiki wa Simba wakimtupia lawama nyingi na kumuangushia laana za kila aina lakini Chuji aliongeze kiwango zaidi ya kile.
Chuji alikuwa tishio anapokutana na Simba kwenye uwanja wa Taifa, alikuwa na vita uwanjani alipokutana na swahiba wake Haruna Moshi ‘Bobani’ na Juma Nyoso.
Chuji alikuwa tegemezi la Yanga na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ iliyokuwa chini ya kocha Marcio Maximo wakati huo. Kila kipindi kina nyakati zake, Chuji ameshamaliza nyakati zake.
Hakuna shabiki wa soka Tanzania kwa sasa asiyemfahamu kiungo wa Simba, Mghana James Kotei kutokana na uwezo wake wa kuukata umeme wa wapinzani unapowaka langoni mwao.
Kotei anacheza kama Chuji, anakaba, anashambulia na anacheza zaidi ya nafasi moja uwanjani. Anaweza kucheza kama kiungo mkabaji, kiungo wa kati na hata beki wa mwisho kwa wakati mwingine.
Kotei akicheza kama kiungo mkabaji anacheza vyema, kiungo wa kati anacheza vyema na akicheza kama mshambuliaji wa kati pia anacheza vyema pia.
Kotei alionyesha kiwango cha hali ya juu kwenye mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Februari 25, mwaka huu pale kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Alianza kucheza kama kiungo wa kati alitibua mipango ya Niyonzima na kumuondosha nje Kamusoko. Pia alicheza kama beki wa kati na alifanikiwa kupoteza ndoto za Chirwa na Msuva.
Hivyo ndio mchezaji kiraka anatakiwa awe, Chuji alikuwa akicheza zaidi ya nafasi moja kama Kotei anavyocheza sasa. Simba haina hofu tena kwa kuwa ina mtu anayehakikisha lango lao halikai wazi.
Kotei alionyesha kiwango cha hali ya juu kwenye mchezo uliochezwa hivi karibuni dhidi ya Mbao. Alisaidia timu yake kupata ushindi wa mabao 3-2 wakitokea nyuma ya mabao mawili.
Kotei alikuwa mmoja kati ya wachezaji watatu waliofunga bao moja kwenye mchezo wa huo uliochezwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.
Kotei amekuwa muhimili muhimu sana kwenye kikosi cha kocha wao, Joseph Omog kwenye kikosi cha Simba na baadhi ya mashabiki wameanza kumfananisha na kiungo wa zamani wa klabu hiyo Mkongo Patrick Mafisango.
Mafisango alikuwa kiungo mahiri kwenye klabu ya Simba ambapo aliisaidia klabu yake kupata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Yanga na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara mwaka 2011.
Mafisango alifariki kwa ajali ya gari mwaka 2012 akitokea kwenye ukumbi wa starehe unaofahamika kwa jina la Dar Live uliopo Mbagala, Dar es Salaam.
AL OROUBA SC
Msimu uliopita alicheza kwenye klabu ya majaribio kwenye klabu ya Al-Orouba inayoshiriki Ligi Kuu ya Oman.
Akiwa amesajiliwa Orouba SC ya Oman, Mchezaji huyo alifanikiwa kucheza mechi nane za Ligi Kuu nchini humo.
Kotei ameanza kuwasahaulisha machungu mashabiki wa Simba baada ya kuondokewa na Chuji miaka 8 iliyopita.
No comments:
Post a Comment