Mshambuliaji Donald Ngoma ameimaliza kabisa hofu ya Yanga hii ni baada ya kuanza mazoezi na kikosi hicho.
Ngoma anaweza kuanza mazoezi abaada ya madaktari waliokuwa wakimtibu goti nchini Afrika Kusini, kumruhusu kuanza mazoezi.
Mzimbabwe huyo, alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha hayo yaliyosababisha azikose mechi za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara na zile za kimataifa.
Kurejea kwa Ngoma kutaiimarisha safu ya ushambuliaji ya Yanga inayoundwa na Obrey Chirwa, Simon Msuva na Amissi Tambwe.
Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa amesema mshambuliaji huyo anatarajiwa kuanza mazoezi wiki hii baada ya kurejea nchini akitokea Afrika Kusini alipokwenda kufanyiwa vipimo vya mwisho kabla ya kuruhusiwa.
Mkwasa alisema mshambuliaji huyo alipumzishwa na madaktari hao kwa muda wa miezi minne ambayo tayari imemalizika, hivyo yupo fiti hivi sasa kwa ajili ya mapambano.
Aliongeza kuwa, timu yao inaendelea na mazoezi ya gym na mazoezi ya uwanjani kila siku asubuhi na jioni kwa muda wa wiki mbili kabla ya kucheza mechi za kirafiki.
"Ni habari njema kwa mashabiki wa Yanga kuwa mshambuliaji wao Ngoma yupo fiti baada ya kupona goti lake. Madaktari wa Afrika Kusini wamemruhusu kuanza mazoezi.
"Anatarajiwa kuanza mazoezi mapema wiki hii mara baada ya kurejea kutoka Afrika Kusini alipokwenda kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya mwisho.
"Kurejea kwa mshambuliaji huyo kutaimarisha kikosi chetu kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii, ligi kuu na michuano ya kimataifa Afrika tutakayoshiriki mwakani," alisema Mkwasa.
No comments:
Post a Comment