Katika
kuadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Disemba, 2016 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d)
ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa
wafuatao:-
(i) Wafungwa wote wamepunguziwa
moja ya sita (1/6) ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la
kawaida linalotolewa chini ya kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58
isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2 (i-xx).
(ii)Wafungwa wagonjwa
wenye magonjwa kama UKIMWI, KIFUA KIKUU
(TB) na SARATANI (CANCER) ambao
wako kwenye “terminal stage”.
Wafungwa ambao wamethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.
(iii)Wafungwa wazee wenye umri wa miaka
sabini (70) au zaidi ambao umri huo umethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya
Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu
wa Wilaya.
(iv)Wafungwa wa kike walioingia na mimba
gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.
(v)Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na
akili (Physical disability and mental
disability) ambao ulemavu huo umethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya
Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga
Mkuu wa Wilaya.
2.Aidha, Msamaha huu wa Mheshimiwa Rais
hautawahusu wafungwa wafuatao:-
(i)Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya
kunyongwa.
(ii)Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya
kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo
gerezani.
(iii)Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha
maisha gerezani.
(iv)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa
makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama
vile cocaine, heroin, bhangi n.k.
(v)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa
makosa ya kujihusisha na uombaji, upokeaji au utoaji rushwa.
(vi)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa
makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda
makosa hayo (robbery with violence,
armed robbery and attempt robbery).
(vii)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa
makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (firearms, ammunitions and explosives).
(viii)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa
makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti, au kujaribu kutenda
makosa hayo.
(ix)Wafungwa waliopatikana na hatia na
kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na
Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na
nane (18) na kuendelea.
(x)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa
makosa ya wizi wa magari na pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo.
(xi)Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya
Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act.
No. 6/2002).
(xii)Wafungwa waliopatikana na hatia na
kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.
(xiii)Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo
na Msamaha wa Mheshimiwa Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya
kifungo kilichobaki.
(xiv)Wafungwa waliopatikana na hatia na
kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.
(xv)Wafungwa waliopatikana na hatia na
kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya
binadamu (Human Trafficking).
(xvi)Wafungwa waliopatikana na hatia na
kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.
(xvii)Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya
kujihusisha na usafirishaji wa nyara za
Serikali na ujangili (Poachers).
(xviii)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa
makosa ya wizi/ubadhirifu wa fedha
za Serikali.
(xix)Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa
makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali.
(xx)Wafungwa
walioingia gerezani baada ya tarehe 9/10/2016.
3.Wafungwa
wapatao 5,678 watafaidika na msamaha
huu baada ya kupunguziwa 1/6 ya
vifungo vyao ambapo 1,340 wataachiliwa
huru na wafungwa 4,338 watanufaika
na kubaki gerezani wakitumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.
Ni
mategemeo ya Serikali kwamba watakaoachiliwa huru watarejea tena katika jamii
kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda
makosa ili wasirejee tena gerezani.
Imesainiwa
na;
Meja
Jenerali Projest Rwegasira
No comments:
Post a Comment