Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, jana
Jumapili alifanya ziara katika Uwanja wa Taifa, Dar kwa ajili ya
kuangalia ukarabati unaofanywa na uongozi wa Klabu ya Simba, kisha
akatoa siku tatu kuanzia jana wawe wameshakamilisha marekebisho hayo
kutokana na kufanya uharibifu wa viti walipocheza na Yanga uwanjani
hapo.
Takribani siku 73 zimepita tangu mchezo wa Ligi Kuu Bara uchezwe kati ya
Simba na Yanga ambao ulizaa uharibifu mkubwa wa uvunjaji wa viti 1,784
uliofanywa na mashabiki wa Simba hali iliyosababisha serikali kutangaza
kuzifungia timu hizo kutumia uwanja huo.
Waziri huyo ambaye alifika uwanjani hapo mapema asubuhi, alianzia
ukaguzi katika chumba maalum cha kamera 119 za ulinzi zilizofungwa
uwanjani kabla ya kuingia uwanjani ambapo alitoa agizo kwa kaimu meneja
wa uwanja, Julius Mgaya baada ya kushuhudia baadhi ya maeneo yakiwa bado
hayajawekwa viti kuwa ndani ya siku tatu wawe wamekamilisha ili apate
kukabidhiwa.
Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mgaya alisema: “Kwa sasa suala la
ulinzi lipo vizuri zaidi kutokana na ubora wa kamera zetu 119 za CCTV
kuwa na uwezo wa kuona popote na kuzoom nje na ndani ya uwanja, pia kwa
ndani ukarabati umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kufuatia uharibifu
uliotokea Oktoba Mosi, mwaka huu na tunatarajia ukarabati huo kukamilika
kabla ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara kuanza hapo Desemba 17,
mwaka huu.
“Licha ya hivyo kuna ukarabati wa milango ya chuma 33 ilikuwa
imeharibika na mpaka sasa milango 13 imeshafungwa. Pia mpaka Machi 3,
mwakani tutakuwa tumeshamalizia sehemu ya zima moto tukishirikiana na
wenzetu raia wa China.”
Naye Nape alisema: “Ukarabati kama mnavyouona unakwenda vizuri, kuna
maeneo viti vilivunjwa na Simba lakini pia yapo maeneo viti vililegea
ambavyo vyote kwa pamoja vinafanyiwa ukarabati ila niseme jambo moja
kuwa tusisubiri hadi Desemba 17, Desemba 13, Jumanne (kesho) nataka kuja
kupokea huu uwanja ukiwa umekamilika.”
No comments:
Post a Comment