Bweni la wasichana wa shule ya sekondari ya Mtwara ufundi iliyoko katika Manispaa ya Mtwara Mikindani limeteketea kwa moto leo majira ya saa moja asubuhi.
Akizungumza katika eneo la tukio kamanda polisi Mkoani hapa Thobias Sedoyeka amesema kwamba majira ya saa moja katika shule ya sekondari ufundi kulitokea moto ambao ulianza kuwaka katika mabweni ya wasichana ambapo mpaka sasa chanzo hakijajulikana na kuongeza kuwa hakuna madhara yoyote yaliyotokea kwa binadamu na makadirio ya hasara ya thamani ya jengo na mali zilikuwemo bado haijajulikana.
Naye
mwalimu wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina la Nanyalika amesema
kwamba alikuwepo eneo la tukio wakati bweni hilo la wasichana wa shule
ya sekondari ya ufundi linaanza kuteketea ambapo kwa upande wake hajui
chanzo cha moto huo hali ambayo imepelekea walimu ambao wanaishi ndani
ya shule hiyo kuwa na hali ya sintofahamu kwa kuhofia usalama wao.
kwa
upande wake mwalimu wa shule ya sekondari Sululu Sekondari iliyoko
Mjini Masasi ambae yupo shuleni hapo kwa ajili ya kusahihisha mitihani
ya kidato cha pili na alikuwa akitumia moja ya chumba cha bweni hilo
amesema kwamba kipindi ambacho wapo katika maeneo yao ya kazi ndipo
walipoona moshi unatokea kwenye bweni.
Naye
mwalimu Masele Francis kutokea shule ya sekondari ya Namwombe iliyoko
katika Halmashauri ya Masasi ameeleza kuwa kipindi ambacho anatoka
bwenini aliona moshi mkubwa hali ambayo ilimpelekea kurudi ndani ili
kuwapa wenzake taarifa.
Aidha
Afisa Habari wa Manispaa ya Mtwara Mikindani Bi.Jamad Omary amewatoa
hofu walimu pamoja na wanafunzi wa shule hiyo na kuwaomba kuwa
wavumilivu katika kipindi hiki kigumu mbali na hayo amewataka wananchi
wa Manispaa ya Mtwara Mikindani kuwa na ushirikiano wa kutosha pindi
kunapotokea tatizo kama hilo na si kuishia kutoa lawama.
Hata
hivyo Kamanda amesema kwamba taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo
ikiwemo chanzo cha moto huo itatolewa baada ya taratibu zote kukamilika.
No comments:
Post a Comment